Sunday, April 22, 2012

Salva Kiir awaondoa wanajeshi Heglig

Wanajeshi wa Sudan Kusini
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir ameamrisha wanajeshi wake kuondoka kwenye visima vya Heglig katika mpaka unaozozaniwa kati yake na Jamuhuri ya Sudan.
Wanajeshi wa Sudan Kusini waliteka eneo la Heglig wiki jana ambapo walilaumu utawala wa Khartoum kutumia mahala hapo kama ngome ya kufanya mashambulio.
Hapo Alhamisi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon alitaja kuwepo kwa wanajeshi wa Sudan Kusin kama kinyume na sheria ya kimataifa.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa ulitaka Jamuhuri ya Sudan kusimamisha mashambulio dhidi ya Sudan Kusini .
Makabiliano kati ya pande zote yalitishia kuzuka kwa vita vingine. Sudan Kusini ilijiondoa kwa Jamuhuri ya Sudan mwaka jana kufuatia muafaka wa amani ulioafikiwa mwaka 2005 baada ya vita vya zaidi ya miongo miwili.
Hapo Alhamisi, Sudan Kusini ilitoa taarifa na kusema haikuwa na haja ya vita na jirani yake na kusisitiza ingewaondoa wanajeshi wake kutoka Heglig pale Umoja wa Mataifa utatuma waangalizi wake.
Awali rais wa Sudan Omar al-Bashir alitishia kuizima serikali ya Sudan Kusini baada ya kupoteza eneo la Heglig ambalo huzalisha zaidi ya nusu ya mafuta ya Sudan.
Chini ya sheria za kimataifa, Heglig ni sehemu ya Jamuhuri ya Sudan japo mipaka kamili ingali kutambuliwa rasmi.

No comments:

Post a Comment