Taswira za Mabweni yaliyoungua moto
--
Na Joachim Mushi,
WANAFUNZI takriban 50 wa Shule ya Sekondari Kidereko wilayani
Handeni hawana sehemu ya kujihifadhi baada ya bweni lao kuteketea kwa moto
pamoja na baadhi ya vifaa vyao vya shule.
Bweni hilo liliteketea kwa
moto hivi karibuni majira ya asubuhi baada ya kutokea kwa hitilafu ya umeme
kwenye bweni hilo
muda ambao wanafunzi wote walikuwa wakiendelea na masomo darasani.
Akizungumza na Thehabari.com eneo la tukio Mwalimu wa
Taaluma wa shule hiyo, Khamis Said amesema vitu vyote vya wanafunzi takribani
50 waliokuwa wakiishi katika bweni hilo
viliteketea kwa moto, yakiwemo madaftari ya wanafunzi, nguo, magodoro na
vitanda vya mbao viliteketea kwa moto.
“Hatukufanikiwa kuokoa kitu maana baada ya kusikika mlipuko
na baadhi ya watu kuona moshi ukitoka ndani ya bweni hilo ambalo muda huo lilikuwa limefungwa tulikuta
moto umesha tanda ndani na ukiwaka kwa kasi jambo hali ambayo ilikuwa ngumu
kuokoa,” alisema Said.
Amesema kwa sasa wanafunzi hao wanasaidiwa na wanafunzi
wenzao kimalazi huku wakiishi kwa shida kutokana na msongamano uliopo baada ya
bweni lao kuteketea kwa moto. “Unajua baada ya ajali walibaki na nguo za shule
walizokuwa wamevaa siku hiyo pamoja na madaftari ya vipindi vya siku hiyo tu, vifaa
vingine vyote viliteketea kwenye ajali hiyo…shule imetoa baadhi ya fedha na
kuwanunulia maitaji kadhaa japokuwa hayatoshelezi” alisema Mwalimu Said.
Hata hivyo alisema tayari uongozi wa idara ya elimu wilaya
ya Handeni umetembelea eneo la tukio na wanafanya utaratibu wa kuwasaidia
wanafunzi hao. Hii ni mara ya pili kutokea kwa majanga ya moto shuleni hapo
kwani mwaka 2000 wanafunzi walichoma ofisi ya Mkuu wa Shule hiyo baada ya
kuzuka kwa vurugu kati yao
na uongozi wa shule.
Habari hii imeandaliwa na mtandao wa habari: www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment