Zitto Kabwe, Mb.
Benki Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi
pekee yenye takwimu zote nyeti na za uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa
hilo. Katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania eneo la Machapisho kuna
Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic
Review) inayotoka kila Mwezi katika Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo
Mwaka (Quarterly Economic Bulletin). Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu
masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi
wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko wa Bei, Mapato na Matumizi ya
Serikali, Mwenendo wa Biashara ya
Kimataifa na Deni la Taifa.
Ukienda kwenye tovuti ya Benki Kuu leo
utakuta Taarifa hizi. Lakini Taarifa hizi zimeishia Desemba mwaka 2011
zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi Novemba na robo ya mwaka
inayoishia Desemba. Ukitaka kujua Bajeti ya Serikali na mwenendo wake
hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba mwaka 2011, miezi sita
nyuma. Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni kuficha taarifa kwa wananchi.
Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani anafaidika na kufichwa kwa
taarifa muhimu kama hizi?
Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa
(Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna
hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu. Niliposikia tetesi
hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kuweza kuwa na
habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011.
Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!
Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.
Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel
imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna
Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa
hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.
Taarifa zinafichwa.
Ndio. Zinafichwa tena makusudi maana
taarifa hizi zipo Benki Kuu. Huu ni uzembe maana Nchi inawalipa
wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono ili wafanye kazi hizi. Benki
Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi kuchapisha Taarifa hizi. Kama
Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi ambao haupaswi kufumbiwa
macho.
Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.
Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano
akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi Serikalini (#OGP), Taasisi
kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo ni nyeti kwa wananchi na
muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali. Rais wa nchi anaongea
Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!
Inaudhi na kukera sana kwenda kwenye
tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za miezi Sita iliyopita. Benki Kuu
hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki kuu kuu. Rekebisheni jambo
hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa Umma ni ufisadi. Haki ya
kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba yetu. Hatutaki
kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.
Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio
ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo
mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na
Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili).
Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba
kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment