WAKATI
kishindo cha shinikizo la kutakiwa kujiuzulu mawaziri nane wa Serikali
ya Rais Jakaya Kikwete kikizidi kurindima, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
amesema Serikali itatoa tamko lake rasmi kesho.
Awali Katibu
wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama aliwaambia waandishi wa habari juzi
usiku kuwa chama hicho kimefanya maamuzi magumu ambayo yangetangazwa na
Pinda mjini hapa jana.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alipoombwa
na waandishi wa habari jana kuzungumzia sakata hilo, hakukanusha wala
kukiri kuwapo kwa azimio hilo zaidi ya kusema wananchi wasubiri hadi
kesho atakapotoa taarifa rasmi. Alipoulizwa kama kuna mawaziri ambao
wameshawasilisha barua zao za kujiuzulu hadi kufikia jana mchana, Pinda
alijibu kwa kifupi kuwa ‘bado hatujapokea, lakini kama wapo watatuletea
tu”. Ingawa Waziri Mkuu hakukiri kupokea barua yoyote, taarifa zisizo
rasmi, zilisema mawaziri watano waliokumbwa na msukosuko huo
wamekabidhi barua zao huku Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami
akikataa kufanya hivyo.
Mwingine ambaye anatajwa kuwa hajawasilisha barua yake, ni Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi. Chami ajitetea
Dk.
Cyril Chami amesema hataandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo na kusema
anawaachia wananchi wapime kama kweli anastahili kujiuzulu ama la. Akizungumza
na Mwananchi Jumapili jana alisema yuko tayari kujiuzulu endapo tu
wananchi na wabunge watampa fursa ya kusikiliza utetezi wake na kama
bado wataona ana makosa,yuko tayari kuachia ngazi. Dk Chami ni mmoja
wa mawaziri ambao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kikao cha Wabunge wa
chama hicho, kimewapa muda hadi kufikia kesho wawe wameandika barua za
kujiuzulu. Kiini cha D. Chami kutakiwa kujiuzulu, ni kauli za Wabunge
wa CCM kuwa anamkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango
nchini (TBS), Charles Ekelege anayetuhumiwa kwa ufisadi. Hata hivyo
Dk Chami alisema hadi jana wizara yake ilikuwa haijapatiwa ripoti ya
Mamati Maalumu ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokwenda kumchunguza
Ekelege katika nchi za Hongkong na Singapore. “Nataka wananchi
wanielewe nitamwajibishaje Ekelege wakati ripoti ya kamati teule ya
Bunge iliyomchunguza mimi sina…ningejengaje hoja kwa Rais bila kuwa na
tuhuma zake?”alihoji D. Chami. Alisema Mkurugenzi wa TBS ni mteule wa
Rais na kuna taratibu zake ambapo taarifa ya kamati hiyo ndiyo
ingeisadia Bodi ya Wakurugenzi ya TBS kumjadili na kupitisha
maamuzi,”alisema. Alifafanua hata ripoti maalumu ya ukaguzi
iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
hawakuwa wamepewa na wamepatiwa siku tatu zilizopita mjini Dodoma. “Bado
najiuliza CAG alikuwa na agenda gani na wizara yangu kwa sababu
hakutupa ripoti yake lakini akawapa baadhi ya wabunge mpaka
tulipofuatulia juzi baada ya kelele za wabunge”alisema. Aliongeza
kusema Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, leo anashutumiwa kwa
kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Hodhi la Mashirika ya
Umma(CHC) bila kufuata utaratibu. “Utashangaa leo Mkulo anashutumiwa
kwa kutofuata taratibu kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa CHC lakini leo
mimi nashinikizwa nimsimamishe kazi Mkurugenzi wa TBS bila kufuata
taratibu,”alisema. Dk Chami alisema amejitahidi kuomba taarifa hiyo
ya Kamati Teule iliyomchunguza Ekelege lakini hadi jana hajapatiwa zaidi
ya kuambiwa ilipelekwa kwa Spika na hajaambiwa baada ya hapo ilikwenda
wapi. Hata hivyo habari za uhakika ambazo gazeti hili inazo ,
zinaonyesha kuwa baada ya ripoti hiyo ya kamati kufika kwa Spika, Spika
naye aliipeleka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Katika kuthibitisha
Wizara ya Viwanda na Biashara haikuwa imeipata barua hiyo, Februari
2,2012 Katibu Mkuu, Joyce Mapunjo alimwandikia barua Katibu wa Bunge
akimkumbusha awapatie ripoti hiyo. Barua hiyo yenye kumbukumbu namba
GA96/352/01 iliyopelekwa kwa Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilila,
ilisema”nimeona nikukumbushe unisaidie ripoti hiyo niweze kutekeleza
maagizo ya kamati”. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Februari 10,2012
Kamati za PAC na POAC na ile ya Viwanda na Biashara zilikutana Dodoma
ambapo Kamati iliendelea kumtuhumu Mtendaji Mkuu wa TBS. Katika kikao
hicho, wizara iliagizwa kuwasilisha kwa CAG ripoti ya idadi ya magari
yaliyokaguliwa na mapato yake, na wizara ikakabidhi ripoti hizo
Februari 15,2012 kwa barua yenye kumb GA.96/352/01. Ni kwa maelezo
hayo, Dk. Chami alidai tangu wakati huo ofisi yake haijawahi kupokea
ripoti nyingine yoyote iwe ya CAG au kutoka kwa Spika zaidi ya kufahamu
kuwapo kwake bungeni wiki hii. Dk Chami alifafanua kuwa kukosekana
kwa ripoti hizo kulimfanya afungwe mikono ya kwenda kwa Rais kumshauri
amuondoe Ekelege kwa kuwa hakuwa na ripoti iliyokuwa ikionyesha tuhuma
zake. Kutokana na msingi huo, Dk. Chami alisema chombo alichobakia
nacho kuchukua maamuzi ni Bodi ya Wakurugenzi ya TBS na bodi hiyo
iliundwa na kuzinduliwa Machi 29, 2012. Dk Chami alisema bodi hiyo
ilikutana Aprili 5,2012 na Wizara yake ikapokea ushauri wa Bodi hiyo
Machi 19,2012 na wakati ripoti ya ukaguzi maalumu wa CAG akiipokea
Aprili 18 akiwa Bungeni Dodoma.
Omari Nundu Kwa
upande wake Waziri wa Uchukuzi,Omari Nundu jana alitumia Bunge kurusha
kombora kwa Kamati ya Mindombinu kuwa imekuwa na taarifa zisizo sahihi. Nundu
alisema taarifa zote juu yake ni za uongo huku akikanusha kwamba
hajawahi kusaini makubaliano (MoU) yoyote kuhusu mradi wa upanuzi wa
Bandari ya Dar es Salaam gati namba 13 na 14.
Ngeleja Waziri
wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa
Sengerema, alipoulizwa na mwandishi wetu kupitia ujumbe mfupi wa
maandishi(SMS) alijibu kwa kifupi ‘Tuziachie mamlaka za maamuzi”. Mawaziri
wanaotakiwa kujiuzulu ili kuinusuru Serikali ni Waziri wa Fedha,
Mustapha Mkulo,Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige. Wengine ni Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro
Nyalandu. Taarifa zilizopatikana juzi usiku zilieleza kuwa katika
kikao hicho, mawaziri hao kwa pamoja waliwekwa katika eneo maalumu na
wakawa wakiitwa mmoja mmoja kwa ajili ya mahojiano na wabunge na baadaye
kupewa msimamo wa chama. Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Waziri
Mkuu akaendesha kikao kingine cha faragha, safari hii kikimhusisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Frederick Werema na Waziri William Lukuvi.
Wengine
walioitwa katika kikao hicho ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM,
Mwigulu Mchemba,Katibu wa Oganaizesheni na Mahusiano ya Nje Januari
Makamba na Katibu wa wabunge wa chama hicho, Jenister Mhagama.
Hata
hivyo mwenye mamlaka ya kuwafukuza Mawaziri kwa mujibu wa Katiba ni
Rais Jakaya Kikwete aliyewateua ingawa hata hivyo badhi ya wabunge
wanamtuhumu Rais kuwa si mtu wa kufanya maamuzi haraka na kwa shinikizo.
Jana
baadhi ya mawaziri wanaotakiwa kuachia ngazi waliingia katika ukumbi wa
Bunge na kukalia viti vyao lakini mara baada ya kuahirishwa kwa kikao,
waliondoka haraka katika viwanja vya Bunge.
Baadhi yao
walipotafutwa kwa simu ili watoe ufafanuzi na msimamo wao kuhusiana na
azimio hilo la CCM, ama simu zao zilikuwa hazipatikani kabisa na zingine
hazikupokelewa, zilikatwa.
Zitto aendelea kutafuta saini
Katika
hatua nyingine,Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema hoja ya
kumpigia Waziri Mkuu kura ya kutokuwa na imani ipo pale pale kama
mawaziri wanaotajwa kwa ufisadi hawatajiuzulu kufikia kesho. “Sisi
tunasema bila kumwajibisha Waziri Mkuu hawa mawaziri waliotajwa
hawatatoka na wasipotoka madudu haya yatarudia…kwa hiyo ni wao mawaziri
kupima na kuwajibika au wamweke reheni Waziri Mkuu,”alisema. Mbunge
huyo alirejea wito wake wa kuwaomba wabunge wenye uchungu na ubadhirifu
na ufisadi waunge mkono utiaji wa saini hizo na kwamba kama mawaziri
watajiuzulu ifikapo Jumatatu, wataondoa hoja hiyo. Kwa upande wake,
Kiongozi wa Kambi rasmi ya upizania Bungeni, Freeman Mbowe alirejea
msimamo wake wa kuomba kufanyiwa mabadiliko ya katiba ya nchi na kanuni
za Bunge ili Spika asiwe anatokana na chama chochote cha siasa. Mbowe
alitoa kauli hiyo kutokana na kile alichodai, hatua ya Spika Anne
Makinda kutafsiri vibaya kanuni za Bunge na Katiba ya nchi ili tu
kuilinda Serikali na Waziri Mkuu wake ili asipigiwe kura ya kutokuwa na
imani. “Mambo ya ajabu sana eti Spika anasema hili zoezi letu ni
batili…sisi tunamshangaa, wanasheria wanamshangaa na hata wananchi
wanamshangaa… anatoleaje mwongozo kwa kitu ambacho hakipo mezani
kwake?”alihoji. Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kanuni
inataka ili hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri mkuu
iweze kufikishwa ofisi ya Spika, ni lazima ipate sahihi za wabunge 70 na
ndicho wanachokifanya.
Wasomi wazungumza
Baadhi ya wasomi
wa Chuo Kikuu wamelitaka Bunge kufuata sheria na kanuni za Bunge kabla
ya kufanya maamuzi hayo kwa sababu mawaziri hao wanaripoti kwa Rais
Jakaya Kikwete na si Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wakizungumza na
gazeti hili kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasomi hao
walisema kuwa, kutokana na hali hiyo wabunge hao wanapaswa kufuata
kanuni ili waweze kutambua kuwa mwenye mamlaka ya kuwaondoa mawaziri hao
ni Rais na si Waziri Mkuu, hivyo basi kumlazimisha aondoke madarakani
ni sawa na kumuonea.
“Mimi naona wanamuonea bure Waziri Mkuu
Pinda, kwa sababu hana mamlaka ya kuwaondoa Mawaziri madarakani badala
yake wanatakiwa kuangalia kanuni kwanza ndipo waweze kufanya
maamuzi,”alisema Profesa Simon Mbilinyi mwasiasa mstaafu nchini.
Aliongeza
kutokana na hali hiyo wabunge hao walipaswa kumuandikia barua Rais
Kikwete na kumtaarifu kuwa mawaziri wake wameshindwa kufanya kazi badala
yake wanatakiwa kuwajibika kulingana na makosa waliyofanya.
Alisema
kutokana na hali hiyo maamuzi ambayo yangeweza kutolewa na rais
yangekuwa sahihi kwa sababu yamefuata sheria na taratibu zilizotungwa na
Bunge.
Alisema kitendo cha wabunge hao kumshinikiza Waziri Mkuu
kujiuzulu au kuwaondoa mawaziri hao ni kinyume na sheria na ni sawa na
kumuonea, jambo ambalo linaweza kumfanya afanye maamuzi bila ya kufuata
taratibu.
Hata hivyo, Profesa Abdalah Safari alisema kuwa wabunge
wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ni wanafiki, na kwamba wanashindwa kufanya
maamuzi mpaka wasubiri nguvu kutoka kwa wapinzani.
Alisema
kutokana na hali hiyo wabunge hao wamepoteza mwelekeo na kwamba wamejaa
woga jambo ambalo limesababisha kuendekeza ufujaji wa mali za umma kwa
makusudi.
Naye Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Matakatifu Agustino cha
Mwanza (Sauti) Dk Charles Kitima amesema mchakato unaofanywa na
wabunge kwa lengo la kumg’oa Waziri Mkuu Pinda sio suluhu ya kutibu
tatizo la uwajibikaji kwa viongozi serikalini.
“Tunalia watu
wajiuzulu wakati tumebaki na mfumo ambao unaruhusu siasa chafu, Mahakama
inaingiliwa katika maamuzi yake Tume ya Uchaguzi haiko huru, hili
haliwezi kuleta mabadiliko sababu Rais atateua mtu mwingine kufanya kazi
hiyo na shughuli zitaendelea kama kawaida”alisema Dk Kitima.
Dk
Kitima ambaye alikuwa akichangia mada katika kipindi cha jicho letu
katika habari kinachorushwa na kituo cha Televisioni cha Star Tv cha
jijini Mwanza jana, alisema njia pekee ambayo inaweza kuleta mabadiliko
ni kubadilisha mfumo utakaowezesha viongozi kuwajibika kwa wananchi.
“Walijiuzulu
Edward Lowasa, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha nini kimebadilika,
rais ameteua wengine matatizo bado yanaendelea serikalini tatizo si watu
bali mfumo uliopo ambao unatoa fursa kwa viongozi na watendaji
kuwajibika kwa waliowateua”alisema Dk Kitima.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema na Habel Chidawali, Dodoma, Patricia Kimelemeta, Geofrye Nyang’oro
Orodha ya wabunge waliosaini:
- 2. Rashid Ali Abdallah – CUF
- 3. Chiku Aflah Abwao- Chadema
- 4. Saluim Ali Mbarouk – CUF
- 5. Salum Khalfam Barwany – CUF
- 6. Deo Haule Filikuchombe- CCM
- 7. Pauline Philipo Gekul- Chadema
- 8. Asaa Othman Hamad- CUF
- 9. Prof.Kuliyokela Kahigi- Chadema
- 10. Naomi Mwakyoma Kaihula – Chadema
- 11. Sylvester Kasulumbayi- Chadema
- 12. Raya Ibrahim Khamis - Chadema
- 13. Mkiwa Hamad Kiwanga - CUF
- 14. Susan Limbweni Kiwanga- Chadema
- 15. Grace Sindato Kiwelu –Chadema
- 16. Kombo Khamis Kombo – cuf
- 17. Joshua Samwel Nassari – Chadema
- 18. Tundu Antiphas Lissu- Chadema
- 19. Aphaxar Kangi Lugola- CCM
- 20. Susan Anselim Lymo- Chadema
- 21. Moses Machali – NCCR Mageuzi
- 22. John Shibuda Magalle – Chadema
- 23. Faki Haji Makame- CUF
- 24. Esther Nicholas Matiko- Chadema
- 25. Joseph Osmund Mbilinyi- Chadema
- 26. Freman Aikaeli Mbowe- Chadema
- 27. Kurudhum Jumanne Mchuchuli – Chadema
- 28. Halima James Mdee-Chadema
- 29. John John Mnyika- Chadema
- 30. Augustino Lyatonga Mrema- TLP
- 31. Maryam Salum Msabaha- Chadema
- 32. Peter Msingwa-chadema
- 33. Christowaja Gerson Mtinda- Chadema
- 34. Philipa Geofrey Mturano- Chadema
- 35. Christina Lissu Mughwai- Chadema
- 36. Joyce John Mukya – Chadema
- 37. Mchungaji Israel Yohane Natse – Chadema
- 38. Philemon Ndesamburo- Chadema
- 39. Ahmed Juma Ngwali- CUF
- 40. Vincent Josephat Nyerere- Chadema
- 41. Rashid Ali Omar- CUF
- 42. Meshack Jeremiah Opulukwa- Chadema
- 43. Lucy Philemon Owenya- Chadema
- 44. Rachel Mashishanga- Chadema
- 45. Mhonga Said Ruhwanya – Chadema
- 46. Conchesta Rwamlaza – Chadema
- 47. Moza Abedi Saidy- CUF
- 48. Joseph Roman Selasini – Chadema
- 49. David Ernest Silinde- Chadema
- 50. Rose Kamili Sukum - Chadema
- 51. Cecilia Daniel Paresso- chadema
- 52. Kabwe Zuberi Zitto- Kigoma Kaskazini
- 53. Magdalena Sakaya – CUF
- 54. Rebecca Mngodo- CUF
- 55. Sabreena Sungura -Chadema
- 56. Hamad Rashid Mohammed- CUF
- 57. Rukia Kassim Ahmed- CUF
- 58. Mustapha Boay Akoonay -Chadema
- 59. Abdalla Haji Ali -CUF
- 60. Khatibu Said Ali -CUF
- 61. Hamad Ali Hamad -CUF
- 62. Riziki Omar Juma -CUF
- 63. Haji Khatibu Kai -CUF
- 64. Anna Marystella John Malack -Chadema
- 65. Hamad Rashid Mohamed -CUF
- 66. Rajab Mbarouk Mohamed -CUF
- 67. Thuwayba Idrissa Muhamed -CUF
- 68. Masoud Abdallah Salum -CUF
- 69. Muhamad Ibrahim Sanya -CUF
- 70. Ali Khamis Seif -CUF
- 71. Haroub Muhammed Shamis -CUF
- 72. Amina Amour Nassoro -CUF
|
No comments:
Post a Comment