Tuesday, May 29, 2012

Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA):'' Tunaomba Waislamu Wote Kurudi Majumbani na Kuendelea na Shughuli Zao za Kawaida za Maisha na Wasijihusishe na Kitendo Chochote Cha Uvunjifu wa Amani Maimamu wote Tunaomba Wawatake Waumuni Wao Kutunza Amani Kama Mafundisho ya Dini Yetu Yanavyotuelekeza ''.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) Muhiddin Zubeir Muhiddin


Watukufu waislam,
Assalamu Alykum Warahmatullah Wabarakatu.
Kwanza kabisa tunataunguliza shukurani kwa Allah (S.W) kwa uwezo wake kutuwezesha kuishi katika visiwa hivi kwa salama na amani licha ya kupita katika mikiki mbali mbali. Aidha sala na salamu zimfikie Mtume Muhammad (S.A.W), Mtume ambaye ametufundisha dini ya amani inayotutaka kuishi kwa amani, mapenzi na umoja katika jamii.
 
Watukufu Waislam,
Kufuatia kukamatwa kwa Sheikh Mussa Juma ambaye ni muhadhiri wa dini ya kiislam hapo jana tarehe 26/05/2012 kumejitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyodaiwa kufanywa na watu wanaotaka kuachiwa kwa sheikh huyo sambamba na matumizi ya nguvu ya jeshi la polisi kukabiliana na watu hao, hali ambayo imesababisha kuvunjika kwa amani, watu kuishi kwa taharuki, khofu kutawala katika jamii, kusita kwa shughuli za maisha kwa wakazi wa Manispaa ya Mjini Unguja pamoja na kusababisha matatizo ya usafiri katika manispaa hiyo.

Katika muktadha huu Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) inawataka waislamu wote kurudi majumbani na kuendelea na shughuli zao za kawaida za maisha na wasijihusishe na kitendo chochote cha uvunjifu wa amani. Maimamu wote tunaomba wawatake waumuni wao kutunza amani kama mafundisho ya dini yetu yanavyotuelekeza. Sambamba na hili maimamu waendelee kuiombea dua nchi kudumu katika usalama na amani.

JUMAZA inawataka waumuni wote wafahamu kuwa kuhusu watu waliokamatwa na kuzuiliwa na jeshi la polisi mpaka sasa, viongozi wa taasisi wa Jumuiya za kiislamu wanafanya kila juhudi kuzungumza na viongozi wa kitaifa na jeshi la polisi katika kulitafutia ufumbuzi suala lililojitokeza na hatua yoyote itakayofikiwa waislamu watajuilishwa.

Wabilahi Tawfiq
Imeandaliwa na;
Muhidin Zubeir Muhidin
Katibu Mtendaji wa JUMAZA

No comments:

Post a Comment