Saturday, May 19, 2012

Dk Kigoda amng’oa kigogo wa TBS






WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda ameiagiza Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake Mkuu, Charles Ekelege.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Kigoda alisema Mkurugenzi huyo wa TBS anatakiwa kusimamishwa kazi ili kupisha taratibu za kisheria ikiwamo suala la uchunguzi dhidi yake kufanyika.


“Moja ya sababu iliyomfanya Rais afanye mabadiliko ya uongozi katika wizara hii ni Shirika la TBS. Kulikuwa na mjadala mkubwa bungeni kuhusu utendaji wake. Nimewataka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo mara moja ili kupisha utaratibu mwingine wa kisheria kuanza.”


Dk Kigoda ametoa kauli hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kuzungumza na waandishi wa habari tangu kuteuliwa kwake na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni.


Wakati akitangaza Baraza hilo, Rais Kikwete alizungumzia azma ya Serikali kuchukua hatua kwa watendaji wengine wa Serikali na taasisi zake ambao alisema ni chanzo cha mabadiliko hayo.


Rais Kikwete alisema mawaziri wamekuwa wakijiuzulu hata kwa makosa ambayo si yao na kwamba Serikali itaanza kuchukua hatua kwa watendaji wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma pamoja na bodi za mashirika husika.


“Pamoja na kuwa na utaratibu huu mzuri wa kuwajibika kwa wanasiasa, sasa lazima tuwawajibishe hata hao wanaosababisha mawaziri hawa kujiuzulu, maana wakati mwingine wanawajibika kwa makosa ambayo si yao,” alisema Kikwete na kuongeza:


“Kuna watu ambao kazi yao ni kupiga fitina tu …wao wana kazi ya kusema kaja hapa ataondoka kwani yeye ni nani bwana ……sasa watu wa aina hii hatuwezi kuendelea kuwavumilia hata kidogo, lazima hatua zichukuliwe kwa watendaji wakuu awe ni katibu mkuu wa wizara, ofisa mtendaji mkuu wa shirika la umma, mkurugenzi wizarani au hata bodi ambazo zinasimamia taasisi hizi.”


Madudu ya TBS
Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe ilimtuhumu Ekelege baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye mpango wa TBS wa kukagua bidhaa.


Filikunjombe alieleza kuwa waligundua madudu baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China.


“Tulikwenda Hong Kong na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini anachokifanya Mkurugenzi (Ekelege) huko nje.”


Kiongozi huyo wa POAC alidai kwamba Ekelege aliwapeleka katika ofisi hewa ambayo baadaye waligundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari.


“Tumekwenda Hong Kong na akatupeleka katika ofisi feki na tulipombana akasema kuwa aliomba kwa muda kuitumia ofisi hiyo,” alisema Filikunjombe.


Mikakati ya Dk Kigoda
Dk Kigoda alisema katika kipindi kilichobaki kabla Rais Kikwete hajamaliza muda wake, watahakikisha viwanda ambavyo vimekuwa havizalishi kama awali zinafanya hivyo ili kuleta maendeleo kwa jamii.


“Hakuna maendeleo ya nchi yoyote duniani bila ya viwanda kwani vijana wengi wataajiriwa hivyo tunahakikisha tunaangalia changamoto ambazo zinawakabili na kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisema na kuongeza:


“Viwanda kama cha Urafiki, korosho na vingine wizara imejipanga kuhakikisha tunaangalia changamoto zinazovikabili ili vianze kutoa huduma kama kawaida.”


Dk Kigoda alisema katika kuleta maendeleo kuna haja ya Serikali kujenga uhusiano wa karibu na wawekezaji kwani kufanya hivyo kutafungua milango kwao kupenda kuwekeza nchini.


“Wizara inajipanga kuhakikisha inapunguza urasimu wa masuala ya kodi kwani hivi sasa mfanyabiashara akiwa na biashara yake ya kusafirisha, atakutana na vipingamizi vingi vya kodi.”


“Hivi sasa mfanyabiashara anayetoa mfuko wa saruji India ni rahisi kuliko kutoa mfuko huohuo kuupeleka Mwanza kutoka Dar es Salaam kitu ambacho ni hatari kwa maendeleo ya nchi.”


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu aliwataka wafanyakazi katika wizara hiyo kila mmoja kufanya kazi kwa nafasi yake kwa kujituma.


Teu alisema hakuna haja ya kufanya kazi kwa kushinikizwa kwani dhamana yao katika taifa na jamii ni kubwa.
“Jamii na taifa linategemea maendeleo na hakuna maendeleo bila viwanda na biashara, hivyo ili wananchi wafurahie matunda yetu ni wajibu wa kila mmoja wetu kufanya kazi kwa kujituma na kwa weledi mkubwa,” alisema                                                                                                                                                                         .KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment