Tuesday, June 12, 2012

Mabilioni ya elimu yateketea, watoto bado hawajui kusoma




RIPOTI ya utafiti, iliyotolewa na Shirika huru la Uingereza la Independent Commission for Aid Impact (ICAI), imeeleza kwamba msaada unaotolewa na Serikali ya nchi hiyo kwa Tanzania, umechangia  kuporomosha kiwango cha elimu katika nchi hizo.

Mbali na Tanzania, ripoti hiyo pia imesema misaada hiyo imechangia kuporomosha elimu kwa nchi za Ethiopia na Rwanda.

Ripoti hiyo ina kichwa cha habari, DFID’s Education Programmes in Three East African Countries, inasema msaada wa Paundi bilioni moja sawa na Sh2.5 trilioni  uliotolewa ndani ya miaka 10, lakini haujazisaidia nchi hizo badala yake watoto wamekuwa wakihitimu elimu ya msingi bila kuwa na msingi wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Kwa mjibu wa ripoti hiyo, Tanzania ni nchi ya pili ambayo inapewa misaada hiyo, Ethiopia  inaongoza na Rwanda ni ya mwisho.

Ripoti hiyo inafafanua kwamba  kufikia mwaka 2014/ 15, Tanzania itakuwa inapokea Paundi 60 milioni  kwa ajili ya bajeti yake, Ethiopia itakuwa ikipokea Paundi 100 milioni na Rwanda Paundi 20 milioni.

Takwimu hizo zinaonyesha fedha zinazotolewa kwa  Rwanda zinapungua, lakini  Tanzania na Ethiopia kinapanda kwa kasi kila mwaka.

Inaonyesha pia mwaka 2011/12 Tanzania ilipokea Paundi 44 milioni  na asilimia 94 zilielekezwa kwenye sekta nyingine na kusaidia bajeti ya Serikali na asilimia sita pekee ilipelekwa kwenye elimu.
Ethiopia ilipewa Paundi 61 milioni na asilimia 51 zilienda kusaidia bajeti ya Serikali, asilimia 45 ilipelekwa kuboresha elimu na maeneo mengine asilimia nne.

Pia inasema Rwanda ilipokea Paundi 24 milioni kwa ajili ya sekta ya elimu na asilimia 98 ilielekezwa kusaidia bajeti ya Serikali wakati asilimia 1.5 kwa ajili ya shughuli za utafiti.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kati ya mwaka 2002 na 2003 Tanzania ilipata takribani  dola 280 milioni za Marekani kwa ajili ya elimu wakati Ethiopia  ilipewa takribani dola 90 milioni za Marekani, Rwanda ni ya mwisho na ilipewa dola 60 milioni za Marekani.

Pia katika  mwaka 2007, Tanzania ilipewa wastani wa dola270 milioni za Marekani, Ethiopia dola 330 za Marekani na Rwanda dola 90 za Marekani na  mwaka 2008, Tanzania ikipokea takribani dola 200 milioni za Marekani, Ethiopia dola 230 milioni za Marekani na Rwanda dola 100 milioni za Marekani.

Uchunguzi umeonyesha kwamba watoto zaidi ya 52  milioni, wanapata elimu kwa sababu ya msaada huo, huku walimu wasio na sifa ya ualimu wakiajiriwa kukabiliana na ongezeko hilo la wanafunzi.

Kutokana na hali hiyo, ripoti hiyo inailaumu Idara ya  Kimataifa ya Maendeleo (DfiD) kwa kushindwa kufuatilia kama wanafunzi wanajifunza au la.

“Kiwango cha elimu ambacho kimekuwa kikitolewa katika hizi nchi tatu, ni cha chini kwa kuwa kinapunguza thamani ya matokeo ya maendeleo kinyume na DfiD’s ilivyokuwa ikitarajiwa,” inasema ripoti hiyo.

Pamoja na hayo ripoti hiyo ilishindwa kuainisha kama DfiD ilifuatilia kama walimu na wanafunzi walikuwa wakiingia darasani.

 “Watoto wengi kujiunga na elimu ya msingi, huku wengi wakiitimu elimu hiyo bila kuwa na msingi wa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, kwa maoni yetu ni matokeo ya matumizi mabaya ya fedha zetu,” inaeleza ripoti hiyo.

Katika kipindi cha mwaka 2005/2015, msaada wa DfiD kwa nchi hizo tatu, unatarajiwa kuwa paundi bilioni moja kwa ajili ya kusaidia bajeti za nchi hizo.

Katika hatua nyingine ili  kukabiliana na hali hiyo, ripoti hiyo inasema mambo kadhaa yanatakiwa kufanyika kwa lengo la kuzisaidia wizara za elimu kukabiliana na tatizo la walimu kutembea umbali mrefu kwenda kuchukua mishahara na kucheleweshewa fedha za ruzuku shuleni.

Ripoti hiyo inashauri unapaswa kufanyika mara kwa mara ili kukabiliana na vitendo vya rushwa na ukiritimba.

Kwa upande wa rushwa ripoti hiyo inaonyesha kuwa Tanzania kuna tatizo kubwa la rushwa kutokana na walimu wengi waliofariki dunia kulipwa mishahara.

Ripoti hiyo inaweka wazi kwamba tatizo lingine ni fedha zinazotolewa sekta ya elimu kutofika shuleni kama ilivyopangwa.

Kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, wafadhili wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ili kufikia lengo la milenia la kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, watoto wote wanaweza kuhitimu shule ya msingi.

Ripoti hiyo inaanisha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2010/ 11, elimu imekuwa ni sehemu kubwa ya misaada inayotolewa na DFiD's na mpaka kufikia mwaka 2014, itakuwa ndiyo eneo kubwa zaidi linalopewa fedha.

Ripoti hiyo iliishauri DFiD kuangalia upya vipaumbele vyake ili ubora wa elimu inayolewa iwe moja ya ajenda zake muhimu katika kutoa misaada yake kwenye elimu katika nchi hizo.

Malcolm Bruce ambaye ni  mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya maendeleo ya kimataifa ya bunge la nchi hiyo limeshauri msaada huo uendelee kutolewa kutokana matatizo hayo.

Naibu Waziri wa Elimu na Mfunzi ya Ufundi Philipo Mulugo anasema taarifa alizopokea katika mikoa mbalimbali zinaonyesha kwamba wanafunzi 5,200 waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, hawajui kusoma wala kuandika.

Wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana walikuwa  983,545,  waliofaulu ni 567,567. Kati yao wasichana walikuwa 278,377 sawa na asilimia 54.48 na wavulana walikuwa 289,190 sawa na asilimia 62.49.

Ripoti ya asasi isiyokuwa ya kiserikali ya mwaka 2010 iliyokuwa na kicha cha habari, Je, watoto wetu wanajifunza?,

inabainisha baada ya ada za shule kufutwa mwaka 2001, uandikishaji wa watoto, uliongezeka kwa asilimia 70 mpaka asilimia 110.

Hali hiyo pia ilijirudia katika utafiti, uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment